Sunday, November 20, 2016

Mvua Kali iliyoambatana na Upepo mkali yaleta maafa wilayani Bukombe kata ya Namonge.


Kata ya Namonge wilayani hapa imekumbwa na maafa baada ya mvua kubwa ya muda mfupi iliyoambatana na upepo mkali ilionyesha majira ya saa 10 jioni siku ya jumatano ya tarehe 16/11/2016 . Mvua hiyo imeezua na kubomoa nyumba 132 ambapo kati ya hizo nyumba 47 zimeharibiwa kabisa, mvua hiyo pia imejeruhi watoto 5 waliyokuwa katika maeneo tofauti ambapo majeruhi wanne wanaendelea na matibabu katika kituo cha Afya cha Uyovu.

Mvua hiyo pia imeharibu miundombinu mbalimbali ya taasisi za serikali ikiwemo Vyumba vitatu vya madarasa, choo cha Walimu, nyumba ya Mwalimu ilipata mtikisiko na kunyanyua paa ambalo tayari limerudishiwa katika Shule ya Msingi Namonge. Aidha Miundombinu  mingine ya taasisi za kidini imeharibiwa na mvua hiyo makanisa  ya TAG, ANGLIKANA na PENTEKOSTE.Vitongoji vilivyoathirika na mvua hiyo ni Namonge A nyumba 66, Namonge B nyumba 36, Kazilambwa nyumba 15 na Mwambakikulu nyumba 15, ghala la kuhifadhia Tumbaku la chama cha Msingi Namonge limebomoka na ghala lingine la mfanyabiashara anayejulikana kwa jina la Masanganya nalo limeezuliwa.

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukombe pamoja na Kamati ya Maafa  wamefika eneo la tukio kujionea hali halisi ya maafa ambapo Ndugu Paul Cheyo  kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Bukombe ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya amewapa pole  watumishi , mabalozi na wananchi wote ambao wameathirika na madhara yaliyosababishwa na mvua hiyo na amewashukuru wananchi kwa kuwa na moyo wa kusaidiana wakati wa matatizo.

Kamari ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bukombe yatembelea Majeruhi kujua hali zao baada ya kupata madhara hayo yaliyoletwa na mvua kali iliyoambatana na upepo mkali.

 Ndugu Paul Cheyo Katibu Tawala wa Wilaya akimuangalia kwa umakini mtoto Timotheo Sospeter mwenye umri wa miaka 13 mwanafunzi wa shule ya Msingi Namonge darasa la 4 ambaye alipata majeraha chini ya kidevu,monomi na kichwani hali yake inaendelea vizuri.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe Ndugu Dionis Myinga akipata maelezo ya hali ya mtoto Daudi Charles mwenye umri wa miaka 6 na jinsi alivyopata majeraha hayo kutoka kwa mama mzazi hata hivyo  hali yake inaendelea vizuri.

No comments:

Post a Comment