Wednesday, November 8, 2017

Bukombe Yaendelea Kung'ara


Bukombe imekuwa katika jitihada za kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa jamii katika sekta mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na kutekeleza mipango ya bajeti.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Halmashauri ya wilaya ya Bukombe imekuwa ya Pili kwa Mkoa wa Geita katika Utoaji huduma bora kwa wananchi kwa kuzingatia Sera,Kanuni, na viwango vilivyowekwa kwa kila sekta ya huduma za jamii hususani katika sekta  za Afya,Maji,Elimu,Barabara na Usimamizi wa Fedha.

Takwimu hizi zimejikita katika matumizi sahihi ya fedha kwa ujumla kwa kutumia taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) ya Mwaka 2015/2016 pamoja na taarifa ya kamati ya Hesabu za serikali za Mitaa.

Katika mchanganuo huo Halmashauri ya wilaya ya Bukombe imeshika nafasi ya pili katika  Mkoa wa Geita kwa jumla ya alama 60.83 ikitofautiana kwa alama 11.94 tu na Halmashauri iliyoongoza Kitaifa yenye jumla ya alama 72.73.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Bukombe anapenda kuwashukuru wananchi wote ambao ndiyo wadau wakubwa wa maendeleo wilayani hapa  katika kufanikisha utekelezaji makini wa shughuli zote za kila siku.
Aidha changamoto hazikosekani hivyo tunaahidi kuboresha huduma bora na za kisasa kwa kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha tunazipunguza kama si kumaliza kabisa changamoto zinazojitokeza kwa sekta zote kwa maelekezo ya serikali ya awamu ya tano.

                 TUSHIRIKIANE WANA BUKOMBE 2017.

IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA TEKNOLOJIA, HABARI NA MAWASILIANO.
BUKOMBE

8/11/2017

No comments:

Post a Comment