Monday, April 3, 2017

Kiasi cha shilingi milioni 11.9 za wanakijiji zajenga vyumba viwili vya madarasa katika shule ya msingi Ihurike wilayani Bukombe




Mkuu wa Wilaya ya Bukombe  Mhe.Josephat Maganga afungua rasmi vyumba viwili vya madarasa   shule ya msingi Ihurike .

Mhe. Maganga amesema amefurahishwa sana na tafsiri nzuri kuhusu Elimu bure ambapo wananchi wanashiriki  kuchangia kwa hali na mali ili kuongeza na kuboresha miundombinu ya elimu.
"Hili ni suala la kujivunia sana, kuona juhudi za serikali zikipata ushirikiano kutoka kwa wananchi, naombeni tusiishie hapa twende hivi hivi na katika miradi mingine ya maendeleo" amesema Maganga.





Aidha pongezi za dhati ziwaendee viongozi wa vijiji, Diwani wa kata ya Ushirombo Mhe.Lameck Warangi na Mbunge wa Bukombe Mhe.Doto Biteko kwakuwa viongozi bora wenye ushawishi mzuri wa kuleta Maendeleo katika Elimu wilayani kwetu, kwa pamoja sasa tuendelee kuwa watu swenye kujivunia maendeleo yetu na kuendelea kushirikiana kuboresha miundombinu yetu ya Elimu na Afya." ameongeza Mhe. Maganga.




Diwani wa kata ya Ushirombo Mhe.Lameck Warangi amedhirisha furaha yake kwa wana Ihurike kukamilisha ujenzi huu wenye thamani ya shilingi milioni 22.9 ndani ya siku 60 ikiwa nguvu za wananchi shilingi milioni 11.9 na Serikali kuu ni shilingi milioni 11.



"Wananchi wangu tuendelee kupambana ili kuleta maendeleo ya kielimu na kiuchumi katika vijiji vyetu nasema haya sababu mwenyeviti kutoka vijiji vingine kwenye kata yangu mpo hapa na mmejionea ujenzi huu wa miundombinu ya elimu niiteni nitakuja , maendeleo ya vijiji vyetu huletwa na sisi wenyewe tuchape kazi na pia tuendelee kumshirikisha Mbunge wetu wa Bukombe Mhe.Doto Biteko katika mikakati yetu ya maendeleo,Mbunge wetu anapenda maendeleo atatusaidia na kutuongoza vyema tumpe shukrani zetu za dhati katika kukamilisha maendeleo haya" amesema Mhe. Warangi



Shule ya Msingi Ihurike ina jumla ya wanafunzi 427, wavulana wakiwa 201 na wasichana 226 na walimu 9, pia ina choo kimoja chenye matundu 4,upungufu ukiwa ni matundu 8 kwa wanafunzi wa kike na matundu 6 kwa wanafunzi wa kiume, huku walimu wakiwa hawana choo kabisa na ni shule inayopakana na hifadhi ya msitu wa Kigosi Moyowosi.


No comments:

Post a Comment